Swahili New Testament Bible

Acts 20

Acts

Return to Index

Chapter 21

1

Tulipokwisha agana nao, tulipanda meli tukaenda moja kwa moja mpaka Kosi. Kesho yake tulifika Rodo, na kutoka huko tulikwenda Patara.

2

Huko, tulikuta meli iliyokuwa inakwenda Foinike, hivyo tulipanda, tukasafiri.

3

Baada ya kufika mahali ambapo tuliweza kuona Kupro, tulipitia upande wake wa kusini tukaelekea Siria. Tulitia nanga katika mji wa Tiro ambapo ile meli ilikuwa ipakuliwe shehena yake.

4

Tulikuta waumini huko, tukakaa pamoja nao kwa muda wa juma moja. Waumini hao wakawa waongea kwa nguvu ya Roho, wakamwambia Paulo asiende Yerusalemu.

5

Lakini muda wetu ulipokwisha tuliondoka. Wote pamoja na wanawake na watoto wao walitusindikiza mpaka nje ya mji. Tulipofika pwani, sote tulipiga magoti tukasali.

6

Kisha tuliagana; sisi tukapanda meli nao wakarudi makwao.

7

Sisi tuliendelea na safari yetu kutoka Tiro tukafika Tolemai ambapo tuliwasalimu ndugu zetu, tukakaa nao siku moja.

8

Kesho yake tuliondoka tukaenda Kaisarea. Huko Kaisarea tulikwenda nyumbani kwa mhubiri Filipo. Yeye alikuwa mmoja wa wale saba waliochaguliwa kule Yerusalemu.

9

Alikuwa na binti watatu ambao walikuwa na kipaji cha unabii.

10

Baada ya kukaa huko siku kadhaa, nabii mmoja aitwaye Agabo alifika kutoka Yudea.

11

Alitujia, akachukua mkanda wa Paulo, akajifunga mikono na miguu, akasema "Roho Mtakatifu asema hivi: `Wayahudi kule Yerusalemu watamfunga namna hii mtu mwenye ukanda na kumtia mikononi mwa watu wa mataifa."`

12

Tuliposikia hayo, sisi na wale watu wengine waliokuwa hapo tulimsihi Paulo asiende Yerusalemu.

13

Lakini yeye alijibu, "Mnataka kufanya nini? Mnataka kuvunja moyo wangu kwa machozi? Niko tayari siyo tu kutiwa ndani kule Yerusalemu, ila hata kufa kwa ajili ya Bwana Yesu."

14

Tuliposhindwa kumshawishi tulinyamaza, tukasema tu: "Mapenzi ya Bwana yafanyike"

15

Baada ya kukaa pale kwa muda, tulifunga mizigo yetu, tukaendelea na safari kwenda Yerusalemu.

16

Wengine kati ya wale wafuasi wa Kaisarea walienda pamoja nasi, wakatupeleka nyumbani kwa Mnasoni ambaye tulikuwa tunakwenda kukaa naye kwa muda. Mnasoni alikuwa mwenyeji wa Kupro na alikuwa amekuwa muumini kwa siku nyingi.

17

Tulipofika Yerusalemu, ndugu waumini walitupokea vizuri sana.

18

Kesho yake Paulo alikwenda pamoja nasi kumwamkia Yakobo, na wazee wote wa kanisa walikuwako pia.

19

Baada ya kuwasalimu, Paulo aliwapa taarifa kamili kuhusu yote Mungu aliyokuwa ametenda kati ya mataifa kwa njia ya utumishi wake.

20

Waliposikia hayo, walimtukuza Mungu. Kisha wakamwambia Paulo, "Ndugu, unaweza kuona kwamba kuna maelfu ya Wayahudi ambao sasa wamekuwa waumini na wote hao wanashika kwa makini Sheria ya Mose.

21

Wamepata habari zako kwamba umekuwa ukiwafundisha Wayahudi wanaoishi kati ya mataifa mengine kuwa wasiijali Sheria ya Mose, wasiwatahiri watoto wao na kwamba wasizifuate mila za Wayahudi.

22

Sasa, mambo yatakuwaje? Ni dhahiri kuwa watapata habari kwamba umekwisha wasili hapa.

23

Basi, fanya kama tunavyokushauri. Tunao hapa watu wanne ambao wameweka nadhiri.

24

Jiunge nao katika ibada ya kujitakasa, ukalipe na gharama zinazohusika, kisha wanyolewe nywele zao. Hivyo watu wote watatambua kwamba habari zile walizoambiwa juu yako hazina msingi wowote, na kwamba wewe binafsi bado unaishi kufuatana na maagizo ya Sheria za Mose.

25

Kuhusu wale watu wa mataifa mengine ambao wamekuwa waumini, tumekwisha wapelekea barua tukiwaambia mambo tuliyoamua: wasile chochote kilichotambikiwa miungu ya uongo, wasinywe damu, wasile nyama ya mnyama aliyenyongwa, na wajiepushe na uasherati."

26

Basi, kesho yake Paulo aliwachukua wale watu akafanya ibada ya kujitakasa pamoja nao. Kisha akaingia Hekaluni kutoa taarifa kuhusu mwisho wa siku za kujitakasa na kuhusu dhabihu itakayotolewa kwa ajili ya kila mmoja wao.

27

Wakati siku hizo saba zilipokaribia kuisha, Wayahudi waliokuwa wametoka katika mkoa wa Asia walimwona Paulo Hekaluni. Wakachochea hasira kati ya kundi lote la watu, wakamtia nguvuni

28

wakipiga kelele: "Wananchi wa Israeli, msaada, msaada! Huyu ndiye yule mtu anayewafundisha watu kila mahali mambo yanayopinga watu wa Israeli, yanayopinga Sheria ya Mose na mahali hapa patakatifu. Hata sasa amewaingiza watu wa mataifa mengine Hekaluni na kupatia najisi mahali hapa patakatifu."

29

Sababu ya kusema hivyo ni kwamba walikuwa wamemwona Trofimo mwenyeji, wa Efeso, akiwa pamoja na Paulo mjini, wakadhani kwamba Paulo alikuwa amemwingiza Hekaluni.

30

Mji wote ulienea ghasia; watu wakaja kutoka pande zote, wakamkamata Paulo, wakamburuta, wakamtoa nje ya Hekalu na papo hapo milango ya Hekalu ikafungwa.

31

Walikuwa tayari kumuua, lakini habari zilimfikia mkuu wa jeshi la Kiroma kuwa Yerusalemu yote ilikuwa imejaa ghasia.

32

Mara, mkuu wa jeshi akawachukua askari na jemadari, akalikabili lile kundi la watu. Nao walipomwona mkuu wa jeshi na askari, wakaacha kumpiga Paulo.

33

Mkuu wa jeshi alimwendea Paulo, akamtia nguvuni na kuamuru afungwe minyororo miwili. Kisha akauliza, "Ni mtu gani huyu, na amefanya nini?"

34

Wengine katika lile kundi la watu walikuwa wanapayuka kitu hiki na wengine kitu kingine. Kwa sababu ya ghasia hiyo, mkuu wa jeshi hakufaulu kujua kisa kamili. Hivyo, aliamuru watu wake wampeleke Paulo ndani ya ngome.

35

Paulo alipofika kwenye ngazi, askari walilazimika kumbeba kwa sababu ya fujo za watu.

36

Kwa maana kundi kubwa la watu walimfuata wakipiga kelele, "Muulie mbali!" ic

37

Walipokuwa wanamwingiza ndani ya ngome, Paulo alimwomba mkuu wa jeshi akisema, "Naweza kukwambia kitu?" Yule mkuu wa jeshi akamjibu, "Je unajua Kigiriki?

38

Kwani wewe si yule Mmisri ambaye hivi majuzi alianzisha uasi na kuwaongoza majahili elfu nne hadi jangwani?"

39

Paulo akajibu, "Mimi ni Myahudi, mzaliwa wa Tarso katika Kilikia; mimi ni raia wa mji maarufu. Tafadhali, niruhusu niongee na watu.

40

Yule mkuu wa jeshi akamruhusu. Hivyo Paulo alisimama juu ya ngazi, akawapungia mkono wale watu na walipokaa kimya, akaanza kuongea nao kwa Kiebrania.

Acts 22

 

 

 

 

HTMLBible Software - Public Domain Software by johnhurt.com

 


Other Items are Available At These Sites: